Usimamizi wa Muda ni kama injini inayowezesha mafanikio yako.



Usimamizi wa Muda ni kama injini inayowezesha mafanikio yako.

Wakati ni rasilimali adimu ambayo tunapewa, na jinsi unavyotumia rasilimali hii inategemea kabisa vipaumbele ulivyojiwekea katika maisha yako.

Kupoteza muda, kiuhalisia ni hali ya kujihisi vizuri kwa muda mfupi, lakini inaweza kuwa mtego unaokuvuta nyuma unapohitaji kuwa mbele zaidi.

Unaweza kuboresha ufanisi wako na kuelekea kwenye malengo yako kwa kudhibiti ni nini unachofanya na wakati gani unafanya.

Kuchukua muda kufikiria jinsi unavyotumia wakati wako ni hatua ya kwanza kuelekea kuwa mbunifu wa maisha yako na kuongeza ufanisi mara moja.

Lakini kwa nini watu hupoteza wakati?

Kwa nini tunachagua kuua wakati wetu kwa sababu ya kusitasita na kufanya shughuli zisizo na tija badala ya kuzingatia kile kilicho muhimu?

Hii ni sawa na kuaacha fursa zipite bila kuzitumia.

Tabia hii ya kupoteza muda inaweza kuwa mzunguko wa hatari. Kile kinachoanza kama mapumziko mafupi kuperuzi mitandaoni kinaweza kuishia kuwa masaa mengi ambayo hautayapata tena kama tunavyofahamu kwamba muda haurudi nyuma.

Unapofanya hivyo, unajijengea kizingiti kwa utaratibu wako wa kazi na kuchelewesha kufanikisha majukumu yako.

Wakati mwingine, majukumu yanaweza kuonekana kama milima isiyovukika, na ndio sababu tunakwepa kuanza.

Badala yake, tunachagua kufanya mambo yasiyo na tija, huku tukipoteza wakati badala ya kukabiliana na changamoto.

Je, unataka kuacha tabia hii ya kupoteza muda?

Kuwa na ufanisi zaidi kwenye majukumu yako ni chanzo cha motisha na utakusaidia kudhibiti wakati wako kwa busara.

Lakini kumbuka, kuwa na ufanisi haimaanishi kujaza siku yako na shughuli nyingi tu.

Hapa kuna njia tatu za kuacha kupoteza muda na kufikia ufanisi zaidi:

Anza na Mambo Magumu Kwanza:

Shughulikia majukumu magumu zaidi kwenye orodha yako au yale ambayo yanakutatiza zaidi. Hii inahitaji nidhamu lakini itaongeza utendaji wako na ufanisi.

Mara nyingine unalazimika kupuuzia namna unavyohisi na inakupasa uanze. Kuwa na ile nguvu ya “potelea pote”, “liwalo na liwe”.

Hakuna mtu anayetaka kufanya kazi ngumu, lakini watu wenye mafanikio wanainua vichwa vyao na kufanya mambo haya magumu bila kujali hisia zao.

Tengeneza Orodha ya Shughuli za Kufanya:

Anza na shughuli ngumu asubuhi kwa sababu huo ndio wakati una nishati zaidi. Kisha, tengeneza orodha ya majukumu kwa siku nzima kulingana na umuhimu na dharura.

Kutengeneza orodha ya kazi za kufanya ni njia nzuri ya kutumia ujuzi wako wa kuandaa na kupanga kazi ili kuokoa muda.

Ni kazi gani unayopaswa kumaliza leo?

Ni vitu gani unavyoweza kuvisubirisha hadi baadaye?

Hata zaidi, ni nini kinachopaswa kufanyika kabla ya muda fulani leo?

Anza na jambo hilo kwanza, kisha endelea chini ya orodha mpaka ufikie vitu visivyo na dharura.

Sasa baada ya kumaliza ule ugumu, orodha yako haionekani kuwa ngumu kumaliza tena.

Panga Mapumziko Mafupi:

Hakikisha unapumzika kwa dakika 10 hadi 15. Chagua shughuli inayokutuliza kwa muda mfupi, na hakikisha hauingilii utaratibu wa wenzako ambao wana kazi muda huo wa mapumziko yako.

Mapumziko ya akili ni muhimu na kwa kweli huongeza ufanisi wako.

Chagua kitu kinachobadilisha fikra zako kutoka kazi unayofanya kwa muda mfupi ambao umeustahili.

Kawaida, binafsi huwa nafanya hivi ili kujipooza kidogo kwenye jambo ninalolifanya.

Huwa naingia kwenye mitandao ya kijamii kuperuzi lakini pia ndio muda ambao naweza kuutumia kuongea na marafiki zangu kuhusu Maisha kiujumla.

Kupoteza muda kunamaanisha kuzuia fursa zako za kufanya mambo zaidi na kuwa bora zaidi ya jana yako.

Watu wenye mafanikio huitumia kila saa kwa faida yao, huku wakitumia kila wakati kwa uangalifu.

Kudhibiti mambo yote yanayokuvuruga kutoka kwenye malengo yako ni msingi wa usimamizi wa muda.

Tambua hili:

"Usimamizi wa muda wenye tija ni tabia unayoweza kujifunza, na inaanza na uamuzi wako wa kuwekeza wakati wako kwa yale mambo ambayo yanahitaji kipaumbele."

Chapisha Maoni

0 Maoni