Mambo 4 kuhusu biashara ambayo yataleta mabadiliko katika biashara yako

Katika pita pita zangu za kila siku na kujifunza kutoka kwa wafanyabiashara walioendelea, nimepata nafasi ya kujifunza mambo manne ambayo yanaweza kuongeza athari uliyonayo pamoja na kukuongezea mapato katika biashara yako.

Ili kuwa tofauti na wengine wanaofanya biashara sawa au zinazoendana, ni muhimu kuwa na mtazamo tofauti juu ya biashara, biashara nyingi zilizofanikiwa ni kutokana na kugundua mambo haya mapema kuliko wengine na kuamua kuyafanyia kazi.

Kama mambo mengine tu, ambayo utayasikia kutoka kwangu au kwa wengine ni vitu ambavyo kila mtu anavijua na anakubaliana navyo. Lakini shida ni mtazamo ambao kiuhalisia kila mtu anao wa kwake, lakini haya mambo utakayoyasoma hapa yatakupa uwezekano mkubwa wa kupata yale mafanikio unayoyahitaji, huu ni ushauri wa kibiashara utakaokuwezesha kupata mafanikio makubwa katika biashara yako.


1. Daima, kuwa na fikra za wazi.

Kwenye biashara nyingi, sifa ya kwanza inayokosekana ni dhamira ya kuwa na fikra za wazi, nimeliona hili kwa macho yangu mwenyewe na sisemi tu ili kuyapamba maneno yangu. Ukweli ni kwamba changamoto nyingi zinazozikumba biashara ziwe ndogo au kubwa, ni ile hali ya kuganda, na kutokaribisha mawazo mapya.

Mara nyingi, nimeona wafanyabiashara wakipiga mawazo yao chini, bila hata kuyafanyia majaribio vizuri. Na matokeo ya hili ni kwamba biashara nyingi zinashindwa kutimiza malengo ya waanzishaji. Lakini habari njema ni kwamba suala hili si gumu kubadilisha kabisa.

Inatuhitaji kuunda njia mpya za kupata mawazo mapya ambayo yatapelekea ufanisi katika biashara zetu, kama unafahamu "CHEMSHA BONGO", hii ni njia mojawapo ambayo inahusisha mtu zaidi ya mmoja, lakini hata kama ni mtu mmoja inaweza kutumika, mawazo YOTE yatakayopatikana inabidi yaandikwe bila upendeleo, la msingi ni kuwa limetolewa na mtu yeyote aliyehusika.

Kupitia njia hii, walau mawazo yamesikilizwa ambapo hiyo ni hatua ya kwanza. Lakini kiini cha tatizo bado kipo pale pale, nacho ni fikra mgando kuhusu mabadiliko. Wafanyabiashara wengi wanahisi watabanwa zaidi na kazi, au uwezekano wa hasara utaongezeka.

Kiuhalisia, mimi naamini tofauti, tukifungua fikra zetu nafasi ya biashara kukua inaongezeka. Uvumbuzi wa njia mpya kwenye kitu chochote hupelekea ufanisi kuongezeka hamna anayebisha kwenye hili. Pia hupunguza "risk" kwenye biashara, sababu jambo la hatari zaidi unaloweza kufanya ni kutokuwa na fikra za wazi, kutokubali mabadiliko, kutokuwa na uvumbuzi, lakini pia kutowavutia wateja wako tena.

Baada ya kutambua umuhimu wa kuwa na fikra za wazi, ni muhimu kuhakikisha unafanya hivyo kadri inavyowezekana, una uwezo wa kubadilisha mazingira ya biashara yako wewe mwenyewe.

2. Angalia namna biashara zingine zinafanya kazi.

Mda mwingi, tunajaribu kutatua changamoto zilizopo katika biashara zetu, bila kuangalia namna biashara nyingine zinavyofanya kazi, kwa maana tunaweza kupata majibu kutoka kwa wengine ambayo yatatusaidia katika biashara zetu,.

Kwa kuangalia nje ya sekta yako, utapata mikakati ambayo haukuwahi kuifikiria hapo kabla ambayo itakuwezesha kufanikiwa. Binafsi nimekuwa nikijaribu njia hii na nimeona matokeo makubwa. Na nimejiwekea maazimio ya kujifunza kutoka kwa wengine, ili kuboresha biashara yangu.

Hii inaweza kuhusisha mambo kama;

  • Kutumia graphics kutangaza biashara yako.
  • Kutengeneza tovuti kwa ajili ya biashara yako.
  • Kuandaa mfumo wa kutoa pointi au zawadi kwa wateja ambao watarudi kununua bidhaa au huduma kutoka kwako n.k

3. Kukutana na watu wengi zaidi.


Watu ambao ni magwiji kwenye biashara wanajua umuhimu wa kutengeneza mahusiano mazuri na watu wengine, kwa maana hao ndio wateja watarajiwa wa bidhaa au huduma zao. Nataka nikupe changamoto kidogo, tengeneza mahusiano m,azuri na watu bila kuwa na nia yoyote ya kuwauzia.

Kumuona kila mtu aliye mbele yako kama mteja, ni sawa na kubeba bango lilioandikwa "NUNUA" chochote ambacho utakuwa unauza.

Jitahidi kujifunza kutoka kwa watu, upate mrejesho wa mawazo yao juu ya bidhaa fulani na pia ndo unazidi kufungua milango ya kukuletea mafanikio katika biashara yako. Kuwa "MDADISI", wafanyabiashara wazuri wote wana sifa ya udadisi, kama hauna sifa hii basi ni vyema kuanza kuifanyia kazi pia.

Na kama point ya juu ilivyosema, jaribu kukutana na watu tofauti ambao wanafanya biashara nyingine tofauti na yako.

4. Tengeneza biashara iliyobeba thamani ya kweli. (La sivyo, hiyo ni biashara bomu)


Kitu ambacho binafsi nimekuwa nikijaribu, ni kutengeneza biashara ambapo wote muuzaji na mnunuaji ni "WATEJA", mara nyingi hili likikosekana basi nafasi ya kufanikiwa kwa biashara hiyo ni mdogo sana.

Swali la kujiuliza wewe mwenyewe ni ?

Kwa namna gani biashara yangu inaweza kuwa MTEJA wa mnunuaji wa bidhaa au huduma zangu ?

Ukifanya mabadiliko haya, tayari unapata nguvu ya ushawishi kwa wateja wako, hii inamaanisha endapo mteja wako ataamua kukuacha basi pia na yeye anakupoteza wewe. Hii ndo THAMANI ya kweli ya biashara na unajenga brand ya biashara yako.

Kwenye ulimwengu wa biashara, hii ndo tunaita kubadilishana thamani, na kuna fursa kubwa hapa ya kuongeza wigo wa biashara yako kwa kuingia mikataba, udhamini au wateja wako kukuletea wateja wengine lukuki kwa kuwaambia kuhusu bidhaa au huduma zako.





 

Chapisha Maoni

0 Maoni