Takribani miaka minne iliyopita, nilikuwa nikiishi kwenye mapambano na nafsi yangu muda wote. Bado hali hii haijanitoka, lakini nimebadilisha mtazamo wangu kwa kuiona hali hii kama fursa ambayo imebeba uzuri ulioje pamoja na neema. Binadamu wote tunapambana kwa namna moja au nyingine, maana hatuna ukamilifu.
Swali ambalo huwa ninaulizwa sana na watu wengi ni;
"Namna gani nitaondokana na changamoto X ?"
Kwenye post hii nitajaribu kuelezea walau kwa uchache kuhusu kujinasua kutoka kwenye changamoto ambazo zinatukumba. Huu ni ushauri ambao ningewapatia wanangu kama tayari ningekuwa na watoto, lakini nitawapatia Mwenyezi Mungu atakaponijaalia neema ya kuwa nao.
Kwa namna flani, huu ushauri sio kwa watu ambao wanapitia changamoto tu, bali kwangu mwenyewe pia kwa maana kipindi cha nyuma, nimepitia nyakati kama hizi za changamoto chungu mzima. Ni ushauri ambao ningetamani kuupata katika nyakati hizi.
Kuna wakati katika maisha, wote huwa tunapata hisia za namna hii, kuzishinda changamoto haimaanishi kuteseka bali kuondokana na ugumu na mzigo mzito ambao umekuelemea. Lengo sio kuepuka changamoto bali kuzikubali na kuzipokea kwa moyo wote, kwa maana zinatujenga. Twende pamoja katika shimo lolote ambalo unajihisi umezama, na tuangalie kama tunaweza kupata kamba ya kutuvuta nje.
Zifuatazo ni dondoo zangu 5 zitakazokusaidia kwenye changamoto yoyote ile;
1. Kuwa Zaidi.
Katika nyakati ngumu nilizopitia, kitu kimoja kilinisaidia sana; nacho ni kutambua kwamba ninapaswa kuwa zaidi ya nilivyo kwa wakati huo. Ukitambua ulipo, na ukaamua kwa dhati kabisa kuwa zaidi, basi mabadiliko madogo madogo yataanza kutokea ndani yako.
Nilikuwa napitia changamoto kwa sababu nilitambua ninaweza kuwa mtu ambaye kila anayenifahamu atajivunia, lakini mwenendo wangu haukuwa ukielekea katika njia hiyo, niligubikwa na upotezaji wa muda wangu wa thamani bila msingi wowote n.k
Kama unapitia changamoto yoyote, kitu unachoweza kufanya ni kuzibeba changamoto zako kama mimi nilivyofanya kwa kuzifanyia kazi. Unatakiwa uazimie kuwa bora zaidi kwenye jamii yako na kujiwekea misingi na imani ya juu kabisa.
Ni kwa kufanya hivi pekee ndio utaweza kujipa heshima wewe mwenyewe lakini pia na familia yako, Baba yangu mzazi alipofariki, nilikuwa mdogo lakini kwa kuwa ni wa kwanza kuzaliwa nilitambua nina jukumu kubwa la kuwaongoza wadogo zangu na familia yangu kiujumla lakini imechukua muda hadi picha hii kukaa thabiti ndani ya akili yangu, nitaifanya familia yangu kujivunia.
Unaweza kuwa zaidi, kama ambavyo unatamani, na ukaleta mabadiliko makubwa kwenye dunia hii. Epukana na uoga wako, uoga wa namna gani wengine watakuangalia, kuishi maisha ya uongo kwenye mitandao ya kijamii na vitu vyote ambavyo kiuhalisia haupendezwi navyo.
Fukia historia yako ya zamani, na chagua kuwa zaidi.
2. Fanya Zaidi.
Wote tuna uvivu yanapokuja mambo ya msingi, kama unahangaika basi ni kwa sababu inakupasa kufanya zaidi ya unayoyafanya sasa. Lakini kuna mambo mazuri na mabaya, ukifanya mabaya zaidi basi mapambano na nafsi yako yatakuwa makubwa zaidi. Inakupasa uongeze juhudi kwenye kuyafanya mambo mazuri kama vile;
- Kuwapa watu tabasamu bila sababu
- Kuwasaidia ambao wana shida na wamekwama katika maisha yao
- Anzisha ile biashara ambayo unaogopa kuianza
- Fanya yale unayoyapenda kutoka moyoni kabisa ili uweze kuishi maisha mazuri
- Tafuta mwenzi atakayekuwezesha kuufurahia upendo wa kweli
3. Furahia Zaidi Wakati wa Sasa.
Kuna msukumo mkubwa sana kutoka kwa jamii yetu juu ya namna tunavyopaswa kuyaishi maisha yetu, ambapo kuna kuzaliwa, kumaliza shule, kwenda chuo, kuoa, kustaafu na mwisho kifo. Ni kweli kuna vitu vya muhimu kuvipata katika wakati sahihi lakini kuishi kwa namna hii ni kupuuzia wakati ulionao sasa na mwisho tunaipoteza ile dhana ya kwamba kila kitu kinachukua muda.
Kitu pekee ambacho tuna uhakika nacho ni pumzi yetu ya sasa, kwenye mazingira yoyote ambayo upo basi ni vyema kutambua kwamba wakati wa sasa unapaswa kupewa nafasi yake katika maisha yako, na kama hali hii hairidhishi basi ndio mwanzo wa kufuata dondoo nambari 1 na 2 kwa kwa kuwa utafurahia mwelekeo wa maisha yako.
Hapa sisemi kwamba usiweke malengo kwa ajili ya kesho yako, laaah ila usiwekeze nguvu nyingi sana kuitazamia kiasi kwamba ukapoteza dira ya baraka ulizonazo katika wakati huu wa sasa. Kuhodhi vitu vingi hakutaleta furaha ya kweli, bali kulitilia maanani kila funzo litakaloletwa na maisha pamoja na safari ya kujitafuta wewe ni nani ndio kutakuletea furaha ya kweli katika maisha.
Kuibadilisha dunia kwa kuanza na wewe mwenyewe, kuwapunguzia wengine kidogo ulichojaaliwa pamoja na upendo wa dhati kwa wengine kutakufanya uwe na amani ya moyo.
Vitu hivi vitakusaidia kutimiza lengo la kuletwa hapa duniani, sote tunaweza kupata ushindi wa kutimiza lengo hili, endapo tutaamini kwamba tuna uwezo na tunastahili kushinda.
4. Safiri Zaidi.
Kusafiri pamoja na kutembea zaidi, kutafungua macho yako na utaziona baraka tele ambazo umejaaliwa kwa maana kuna watu wenye changamoto nyingi zaidi yani wewe haufui dafu kwao. Katika safari zako, utaona watu ambao si tu mafukara, bali waliopoteza akili zao na wengine wakitamani tu kufa.
Fungua macho yako kuona uzuri wa asili ambao unakuzunguka, usichukulie poa. Kuna mito, mabonde, jamii mbalimbali za wanyama na miti. Ukiangalia vitu vyote hivi kwa jicho la tatu, akili yako itafunguka zaidi na kukuwezesha kuwa kiumbe bora kabisa.
Changamoto hazikupotezi mazima, bali ni kwa muda mfupi tu. Na ni wakati huo huo inakupasa utafute suluhu ya changamoto zako, inakubidi ujitafute na kusafiri kwenda sehemu tofauti ni njia mojawapo ya kufanya hivyo.
5. Pambana Pamoja na Wengine.
Umoja ni nguvu, na utengano ni udhaifu.
Hakika wahenga hawakukosea kusema hivi, angalia ni wakina nani wamekuzunguka ?, nani atakufaa katika dhiki ?. Ila kama unapambana jibu ni kwamba hamna msaada mpaka umefikia hali hiyo, ili kurudi kutoka kwenye shimo la ugumu na taabu inabidi uruhusu wengine wakusaidie.
Wachache sana watatoa msaada huu bure, inabidi ukubaliane na hilo. Lakini njia nzuri zaidi ni kutoa kabla ya kuwavutia watu sahihi, tukiangalia kwa mfano kampuni ya AZAM kwa namna yoyote ile isingeweza kufanikiwa bila ya kuwa na watu ambao wanafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha inafanikiwa.
Mapambano unayopitia ni kwa sababu haujatengeneza msingi imara wa watu ambao watasimama pamoja na wewe kuhakikisha mambo yako yanaenda vizuri. Ili kuepukana na changamoto unahitaji kuwavutia watu sahihi kwenye maisha yako yako ambao wana uwezo wa kubadilisha fikra zako, unahitaji watu ambao watakwambia ukweli unapozingua lakini wengi tunafeli hapa kwa kutaka kuwa karibu na watu ambao wanatupamba kila wakati.
Hakuna marefu yasiyo na ncha, hata shida na tabu zako zina kikomo. Hatuwezi kuzikimbia kabisa changamoto katika maisha ila tunaweza kuwakaribisha wengine watusaidie kwenye kuzitatua na tukashinda vita pamoja, na sisi pia tuwe tayari kupambana vita za hawa watu wetu wa karibu.
Una uwezo mkubwa sana ambao umeufukia, kama lengo langu ni kukujulisha juu ya kuzikubali changamoto na kutokuzikimbia, basi nimefanikiwa.
Rudia baada yangu;
"Nina uwezo wa kuibadilisha dunia"
"Mapambano yananijenga"
"Maumivu ni kitu cha muda mfupi"
"Natakiwa nitengeneza tabia ya kutoa"
"Nitakuwa na imani ya kweli na uwezo wangu"
HATUA GANI INAFUATA BAADA YA HAPA;
Amua sasa kuwa kesho yako inaenda kuwa tofauti, kwa sababu tayari upo kwenye usukani na umeshapata mafunzo ya udereva bora. Geuza picha uliyonayo katika akili yako kuwa changamoto unazopitia ni njia ya kukujenga kuwa bora zaidi.
Binafsi, nilipopitia kipidi hiki niliazimia kubadilisha maisha yangu na nilianza kujifunza kadri nilivyoweza juu ya njia za kujiingizia kipato, kusoma vitabu vingi zaidi kutoka kwa watu waliobobea kwenye fani mbalimbali, nilibadilisha mlo wangu kuwa wenye kunijenga afya yangu iwe imara zaidi, niliamua kutokuwa wa kawaida (MEDIOCRE), na nikasema kwamba NITAIBADILISHA DUNIA.
Mchakato wa mabadiliko ni mgumu sana, lakini hata maisha pia hayakutengenezwa kuwa rahisi, ila unajua utamu wake ni pale unavuka changamoto, ni pale unapofika juu ya mlima mmoja na kukutana na mlima mkubwa zaidi mbele yako na hauna budi kuuvuka.
Elimu hii adhimu inatosha kwa leo ndugu yangu mpendwa, haya ufanye tulivyokubaliana na Mungu akipenda tutakutana kwenye somo jingine.
0 Maoni